Katika juhudi za kuwezesha vijana wa maskani kimafunzo na kazi, Shirika la Sambasports youth agenda limeleta pamoja wafanyibiashara 20, wenye uzoefu wa kazi za kiufundi kuwafunza vijana hao.
Mafunzo hayo ya mradi wa shared Futures unaolenga kubadilisha maisha ya vijana kwa kuwapeusha na magenge na ushawishi wa itikadi kali na utumizi wa mihadarati unatarajiwa kuwapa vijana hao utaalamu wa kazi za kiufundi.
Wafanyibiashara hao wamekubali ushirikiano na Sambasports kuwafunza vijana hao kwa miezi mitatu na zaidi ikitegemea na mafunzo aliyochagua mwanafunzi.
Wakijadiliana wao kwa wao,wafanyibiashara hao kutoka likoni hadi Ukunda, wameelezea changamoto za vijana ikiwemo kukaa ovyo maskani, ukosefu wa malezi bora ya kidini, umaskini, ukosefu wa elimu, utumizi wa mihadarati miongoni mwa changamoto zinazochangia wengi kujihusisha na uhalifu na vurugu.
Kwa kauli moja kupitia mapendekezo yao baada ya kujadiliana wamekubali kuwapokea vijana watakaotumwa kwenye kazi
Miongoni mwa kazi watakazojifunza vijana kutoka maskani 9 kuanzia Likoni hadi Ukunda, ni fundi cherahani, fundi mfereji, uchoraji na upakaji rangi, uchomeleaji wa vyuma, kazi za salon,kinyozi, na useremala.
Akizungumza katika mkutano huo,mshauri wa shirika la sambasorts Mohammed Mwachausa, ameelezea kuwa ushirikiano huo utasaidia pia wafanyibiashara wanaotaka kupokea mafunzo ya mauzo ya bidhaa ama huduma zao, kupata vyeti kutoka kwa vyuo vya kiufundi kwa wale ambao hawana, kulipiwa ada za mitihani katika vyuo vya kiufundi,mafunzo ya mbinu za kufanya biashara na namna ya kutoa maelezo kuhusu biashara zao.
Mwachausa ameongeza kuwa mfumo kama huu umetumika katika kaunti za Lamu, Mandera na Garisa na ulisaidia vijana zaidi ya 5000 kubadili maisha yao.
Mradi wa shared Futures, unatekelezwa na sambasports kwa ushirikiano na AYT kwa udhamini wa Kerk in Actie na ICCO.
Mwandishi: Amina Chombo
Hongera kwa vijana hao na kwa shirika la SambaSports Youth Agenda katika swala zima la kukuza ujasiriamali.