Hatimaye mafunzo ya kazi za kiufundi kwa vijana wa maskani Tisa (9) teule kuanza hivi karibuni. Hii ni katika juhudi za Shirika la SambaSports Youth Agenda wakiwa na washirika wao AYT kuwezesha vijana wa maskani kimafunzo na kazi.
Mapema hii leo , vijana 30 wakiwemo wa kike na kiume walijitokeza ili kufahamu zaidi kuhusu mafunzo hayo ambayo yanatarajiwa kuanza tarehe 24 mwezi huu.
Wafanyibiashara wa idara mbalimbali waliokubali ushirikiano na SambaSports ili kufanikisha zoezi hilo la mafunzo kwa vijana hao kwa miezi mitatu nao pia walihudhuria kikao hicho cha leo ambapo waliweza kuwaelezea kwa ufasaha vijana hao kuhusiana na kazi za kiufundi walizochagua kupata mafunzo.
Mafunzo hayo ya mradi wa Shared Futures unaolenga kubadilisha maisha ya vijana hao kwa kuwaepusha na magenge ,utumizi wa mihadarati pamoja na itikadi Kali na kuwapa ujuzi wa kazi mbalimbali ili kuweza kujikimu kimaisha.
Akizungumza katika kikao hicho afisa mkuu wa Shirika la AYT bwana Yakub Athman aliwasihi vijana hao kua wawe makini katika kuchagua kazi za kiufundi wanazotaka kufunzwa na kutia bidii ili kuweza kupata ujuzi ambao utawafaidi wao wenyewe.
Pia aliwaambia waandike barua za kuomba kushirikishwa kwenye mafunzo hayo na kuonyesha kwamba wamejitolea kikamilifu na sio mguu mmoja ndani na mwengine nnje.
Wakati huohuo aliwaomba wana biashara kuwasilisha mahitaji yao yanayotakikana kufikia jumatatu hii ijayo ili mafunzo hayo yafanyike.
Afisa huyo aliwaahidi vijana hao kua usalama wao wanapokua sehemu hizo ambazo watapokea mafunzo utasimamiwa na mashirika hayo mawili.
Hata hivyo vijana hao waliomba kuongezewa wakufunzi zaidi, vifaa vinavyohitajika na pia kupata vyeti baada ya mafunzo hayo kukamilika.
Miongoni mwa kazi watakazojifunza vijana kutoka 9 kuanzia Likoni hadi Ukunda, ni fundi cherehani, fundi mfereji, uchoraji na upakaji rangi, uchomeleaji wa vyuma na kazi za salon.
Mradi wa Shared Futures, uatelekezwa na SambaSports kwa ushirikiano na AYT kwa udhamini wa Kerk in Actie na ICCO.
Mwandishi: Nrasiku Mwadama